Unawezaje kupata pesa au faida kwa kumiliki blogu?
Published by uhakika media
Unataka kutenegeneza pesa kirahisi sio?, bila shaka, kila mtu anataka kutengeneza pesa halali imsaidie kusukuma maisha yake ya kila siku. Pengine umewahi sikia kuwa ukimiliki blogu ama tovuti unaweza kutengeneza pesa kirahisi?, ndio yawezekana kutengeneza pesa kirahisi kwa kutumia blogu, ila usiwe na shauku sana maana si rahisi tu. Wasomaji wangu wengi wamenitumia ujumbe na wengine kunipigia simu kuuliza nawezaje kupata pesa nikiwa na blogu yangu? Leo nitakushirikisha baadhi tu ya mbinu zinazotumika kupata pesa, na pia mambo muhimu unayopaswa kuyazingatia ili kufanikisha hilo.
Wengi wakiniuliza swali hili, huwa napata picha kwamba, wanahisi blogu ni kama kitu ambacho ukiwa nacho tu chenyewe kinafanya kazi hiyo ya kutengeza faida, na wengine hudhani, pengine walipotoshwa kuwa anaweza anzisha blogu na kuanza kupata pesa bila yeye kama mmiliki wa blogu kuweka juhudi zozote zile!, Hapana, tena ukiwa bloga mpya ndio inakuwa ni ngumu zaidi kupata faida, tazama orodha hii ndogo ya mambo ambayo unapaswa kufanya:
- Andaa na anzisha blogu yako
- Anza kuandaa na kuchapisha maudhui muhimu kwenye blogu yako
- Tafuta wasomaji na wafuatiliaji wa blogu yako
- Jenga mahusiano na ushiriki na wasomaji wa blogu yako
- Weka mifumo mbalimbali ya kupata pesa kupitia blogu yako
Unaona?, kupata pesa ni jambo la mwisho kabisa katika hatua hizo, ila kwa sababu ni hatua tano unaona ni kama rahisi sio?, nitazielezea zaidi hizo hatua ili upate kelewa juhudi unazotakiwa kuwekeza.
1. Andaa na anzisha blogu yako
Ndio, ni lazima uwe na blogu, na uwe unaimiliki wewe mwenyewe, inaweza kuwa rahisi kujifunza jinsi ya kuanzisha blogu kwa kusoma bandiko hili. ambalo ndilo limefanya niulizwe mswali mengi sana kuhusu faida.
2. Anza kuandaa na kuchapisha maudhui muhimu kwenye blogu yako
Blogu haina maana yeyote kama haina maudhui, maudhui(Content) ndio kitu pekee kitakacho tofautisha blogu yako na blogu zingine mtandaoni, maudhui ndio yatakayo kupatia wasomaji na wafuatiliaji wakudumu na hata wapya kwenye blogu yako.
Kimsingi hili ndio jambo la muhimu sana kuzingatia, mfano mwandishi wa habari ana nafasi nzuri ya kuwa na mudhui kwa sababu anakua na habari mpya kila mara, namna atakavyoziandaa habari zake na kuzichapisha kwa wakati inampa fursa kutumia blogu kuwafikia watu wengi kwa urahisi zaidi na wengi watapenda kuarifiwa punde tu unapochapisha habari mpya.
Chochote unachotaka kukizungumzia kwenye blogu yako chaweza kuwa ni kinalenga jamii fulani, au kundi fulani mfano watoto, vijana, wazee, wakulima, wanafunzi nakadhalika, jitahidi kiwe ni bora na chenye upekee. Maudhui mazuri na yenye muelekeo chanya yatawafanya wasomaji wako wajihisi kukufahamu na kukuamini sana hivyo kukuwekea mazingira bora zaidi ya kupata pesa baadae kupitia blogu yako.
3. Tafuta wasomaji na wafuatiliaji wa blogu yako
Blogu yako ni mpya, hakuna mtu anaifahamu na unaamini una maudhui mazuri, sasa weka juhudi ya kuwapata wasomaji na wafuatiliaji, unatakiwa kuitangaza blogu yako. Muhimu hapa ni kujua ni watu gani (type of people) unaotaka wawe wasomaji na wafuatiliaji wa blogu yako. Kwa mfano umeandaa blogu ya mapishi!, ukishafahamu wasomaji wako ni watu wanaojihusisha na mambo ya mapishi basi fuatilia aina hii ya watu inaweza patikana wapi mtandaoni. Andaa orodha fupi yenye vitu kama:
- Je!, wanafuatilia blogu zipi zingine zinazofanana au tofauti na maudhui ya blogu yako?
- Wanashiriki kwenye majukwa gani mtandaoni? mfano (JamiiForums)
- Kuna vipindi vya radio ama tv wanaweza kuwa wafuatilia pia?
- Wanatumia mitandao ipi ya kijamii? orodhesha walau mitatu mikuu
- Wanafuatlia watu gani kwenye hiyo mitandao ya kijamii?
Kwenye maeneo hayo utakayobainisha wasomaji unaowahitaji wanaweza kuwepo, wanaweza kuwa wanashiriki kwa kuchangia maoni na kulekezana. Hivyo na wewe inafaa uanze kuwa mshiriki wa maeneo hayo pia ili wakufahamu na pengine unaweza kutumia mwanya huo kuwajulisha na kuwakaribisha kuangalia blogu yako.
Muhimu ni kujenga uwepo wako, ufahamu, na kuchangia/kuongeza dhamani, epuka kuonekana kama mkorofi wa mtandaoni (spammy) kana kwamba unalazimisha watu wajue blogu yako tu, lakini wala huchangii mambo ya msingi wala kushauri.
Pia bila ushiriki wako, unaweza kuandaa bajeti ya matangazo na kutangaza blogu yako kwenye maeneo hayo ili ipate kufahamika.
4. Jenga mahusiano na ushiriki na wasomaji wa blogu yako
Kwa kuzingatia hizo hatua hapo juu, utakuwa na blogu nzuri, yenye maudhui sahihi na bila shaka umeanza kupata wasomaji, sasa unapaswa kujenga mahusioano ya karibu na wasomaji wako ili waendelee kubaki na pia kukuletea wasomaji wapya.
Jibu maswali yao wanayouliza kuhusu mada husika kwa wingi kadri unavyoweza, pia wasiliana na baadhi yao wanapohitaji mawasiliano nawe kwa njia ya barua pepe nakadhalika.
Kushirikiana na wasomaji ni njia nzuri kukuwezesh akuapata pesa kupitia blogu yako.
5. Weka mifumo mbalimbali ya kupata pesa kupitia blogu yako
Sasa, umeshafanya yote yamsingi, lakini kupata pesa bado, na unahitaji kujaribu na kujuhudi njia mbalimbali kupata pesa. Bado safari ya kujifunza inaendelea, kuna njia nyingi sana za kupata pesa, ila hapa nitorodhesha chache ambazo mimi binafsi huwa nawashauri watu kuzitumia, tena ni njia ambazo bloga wengi huzitumia kupata pesa. Tuanze kujifunza njia hizi:
Kupata pesa kupitia matangazo ya CPC au CPM
Hii ni njia kuu ambayo hutumiwa sana na wamiliki blogu kupata pesa kwa kuweka matangazo madogo madogo kwenye kurasa za blogu zao, ziko aina mbili;
- CPC/PPC – Cost per Click (au Pay Per Click), matanagazo ambayo yanakuwepo kwenye kurasa au pembeni mwa kurasa ya blogu yako yatakuingizia pesa kila msomaji atakapo gonga (click) tangazo hilo.
- CPM – Cost per 1000 Impressions, yani kadiri tangazo litakavyoonekana mara nyingi katika nyakati tofauti tofauti na wasomaji tofauti tofauti utapata pesa kutoka kwa anayetangaza.
Google Adsense ndio mtandao maarufu wa kuchapisha na kupachika matangazo ya namna hii kwa wamiliki wa tovuti na blogu mbali mbali duniani, na inawalipa wamiliki wa blogu hizi vizuri kadiri blogu husika invyofaya vizuri kuzingatia hatua tulizojifunza awali, matangazo yanayopachikwa huteuliwa kielectroniki kuendana na maudhui, pia lugha ya blogu yako.
Uza matangazo binafsi
Ukiwa na watembeali wengi wa blogu yako kwa siku, sio lazima kutumia mitandao ya matangazo kama Google Adsense, Badala yake Makampuni yanaweza kukufuata moja kwa moja kutaka uwatangazie biashara zao. Unaweza pia kuwasiliana na wahusika moja kwa moja, na kwa kuwa hakuna mtu wa kati, hii inakuwezesha kuweka viwango unvyotaka kutoza kwa kila tangazo na ukapata faida kubwa zaidi.
Tangazo linaweza kuwa mfumo wa picha, video, an au hata chapisho zima kuhusu bidhaa fulani, nakadhalika.
Uza bidhaa za kidigitali
Ikiwa hutaki kuhangaika kutangazia watu wengine, unaweza kutumia blogu yako kutangaza na kuuza bidhaa za kidigitali mfano vitabu, picha, muziki, video n.k.
Unachotakwa kuzingatia hapa, bidhaa utakazoziuza ziandane na maudhui ya blogu yako na pia mahitaji ya wasomaji wako, hutakiwi kuacha kuandika mambo muhimu kwenye blogu yako na kufanya biashara tu, kumbuka watu wanafungu ablogu yako kujifunza, hivyo biashara iwe ni jambo la ziada ili wasomaji wako wasichukizwe na waendelee kufurahia blogu yako.
Andaa unachama wa kulipia kwenye blogu yako
Unaweza kuwa mbunifu zaidi na ukaandaa uanachama wa wasomaji wako ambao watajisajili na kulipia ili kupata huduma na maudhui ya kipekee zaidi, mfano mwandishi wa habari anaweza kuwalipisha wasomaji wake kupata habari mahususi zenye kuchambuliwa kwa kina na hata kushuhusia mahojiano aliyoandaa na baadhi ya watu mashuhuri.
Jenga jina na hadhi ya weledi wako
Blogu inaweza kuwa ni njia ya wewe binafsi kuonyesha uwezo na ufanisi ulionao katika fani mbalimbali na hivyo ukapata mialiko ya kufanya mafundisho, ama kupata kazi za kimikataba ambayo utakubaliana na wateja wako wakulipe.
Nimatumaini yangu nitakua nimejibu baadhi ya maswali kwenye chapisho hili, tadhali usiache kujifunza na kuuliza kama una swali jingine, nami nitakuwa huru kukujibu bila shaka.
Nitanendelea kushirikisha taarifa muhimu na mbinu mbali mbali zinazohusu TEHAMA kwa ujumla, hivyo shirikisha bandiko hili na mengine mengi ili nipate wasomaji wengi zaidi kama wewe na hatimae kuongeza ufahamu wa mambo haya katika jamii yetu.
Shirikisha:
Maoni
Chapisha Maoni