Uhakika media 5 · 1 hour ago
Baba Askofu Dkt. Fredrick Shoo,
Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT)
S. L. P. 3033
ARUSHA.
Mheshimiwa Baba Askofu, Shalom!
YAH: MAMBO MATANO AMBAYO HAYAPONYI KATIKA WARAKA WA MAASKOFU WA KKKT
Jina langu ni Kitila Mkumbo, muumini katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), ambalo wewe ndiye mkuu wake. Kikazi, mimi ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Dodoma. Kitaaluma, mimi ni mhadhiri mwandamizi katika Saikolojia na Elimu nikiwa na cheo cha Profesa mshiriki katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Mheshimiwa Baba Askofu, kwa unyenyekevu mkubwa nimeamua kukuandika barua hii ili kutoa maoni yangu binafsi kwa kanisa unaloliongoza kupitia kwako kuhusu maudhui ya waraka uliotolewa na waheshimiwa maaskofu wa KKKT siku ya Jumamosi tarehe 24 Machi 2018. Waraka huo ulitarajiwa kusomwa katika makanisa siku ya Jumapili tarehe 25 Machi 2018. Katika kutoa maoni yangu kuhusu waraka huo, ninalenga mambo makubwa mawili ambayo ni pongezi kwenu, na pili ni mtazamo wangu juu ya baadhi ya masuala yaliyomo katika waraka huo.
Mheshimiwa Baba Askofu, kwa dhati kabisa ninawapongeza sana kwa kujali na kwa utayari wenu katika kuzungumzia na kuchambua kwa kina mambo muhimu ya kijamii, kisiasa na kiuchumi yanayogusa moja kwa moja uhai na haki za kibinadamu za waumini wa KKKT na Watanzania kwa ujumla.
Aidha, ninawapongeza sana kwa ujasiri na kwa kutumia vizuri nafasi zenu katika kanisa na jamii ya Watanzania katika kuyatolea kauli mambo yanayogusa masilahi mapana ya nchi yetu.
Kupitia waraka huo, mmetimiza ipasavyo majukumu yenu ya msingi kwa jamii. Binafsi ninaamini kuwa pamoja na kwamba ninyi ni viongozi wa kiroho, bado mnayo nafasi kubwa katika kuchangia maendeleo ya nchi yetu kisiasa, kijamii na kiuchumi kwani mambo yote hayo yana uhusiano wa moja kwa moja na afya ya kiroho.
Mheshimiwa Baba Askofu, mbali ya pongezi hizo, nina maoni kwenu ninyi viongozi wetu wa kiroho katika mambo kadhaa yaliyobainishwa kwenye waraka, ambayo ninaona kuwa maudhui yake hayaakisi hadhi na wajibu wa msingi wa kanisa.
Kama ambavyo mmekuwa mkitufundisha siku zote, na vile tusomavyo katika Biblia Takatifu, ninafahamu kuwa kazi za msingi za kanisa ni zile ambazo Bwana Yesu Kristo alizifanya alipokuwa duniani. Kazi hizo ni kuhubiri habari njema (injili), kufundisha waumini ambao ni sehemu ya jamii na kuponya wenye shida mbalimbali kijamii, kimwili na kiroho.
Ninaamini kuwa ninyi viongozi wetu wa kanisa ni warithi wa kazi hizo wenye wajibu wa kuziendeleza hapa duniani. Inatarajiwa kuwa maneno na matendo yenu ndani na nje ya kanisa yatakuwa yenye mwelekeo wa kutekeleza kazi hizo ambazo matokeo yake ni uponyaji wa jamii na kuleta matumaini ya kimaisha, kiroho na kimwili.
Mheshimiwa Baba Askofu, katika waraka wenu mmetoa maoni katika maeneo 18 ambayo mmeyagawanya katika maeneo makuu matatu (jamii na uchumi; maisha ya siasa na masuala mtambuka). Kwa ujumla, ninakubaliana na mengi mliyogusia katika waraka huo na ninaamini yamefundisha na kuponya roho zetu kwa kiasi kikubwa, hasa kipingele cha tano (v) mnapozungumzia masula mtambuka pale mnaposema: “Uhai wa mtu una thamani isiyopimika. Ni wajibu usiokwepeka kuulinda na kuutunza uhai kwa vitendo halisi. Endapo uhai umepotea katika mazingira yoyote, uchunguzi huru na wa haki ufanyike na taarifa zitolewe kwa wakati muafaka ili kujenga jamii yenye imani kwa Serikali na vyombo vyake”.
Hata hivyo, yapo maeneo matano (5) muhimu mliyoyatolea kauli ambayo, kwa maoni yangu, hayaponyi bali yanaleta mkanganyiko zaidi kwa jamii kwa kuwa hayakujengwa katika msingi wa mantiki na ushahidi wa neno la Mungu, wala kuzingatia mantiki na ushahidi wa kisayansi, ambayo siku zote yamekuwa ni msingi wa hoja za KKKT.
Mheshimiwa Baba Askofu, baada ya maelezo hayo ya utangulizi, naomba sasa niyabainishe maeneo hayo matano ambayo ninaamini kuwa mngejipa nafasi ya kutafakari kwa kina zaidi msingeyatolea kauli au mngeyatolea kauli kwa namna nyingine.
1.Kuhusu uhuru wa Bunge, Mahakama na Tume ya Uchaguzi
Mheshimiwa Baba Askofu, katika kujadili maisha ya siasa, katika hoja yenu ya nne (4), mmeeleza kwamba kuna “kubanwa na hatimaye kuelekea kupungua kwa uhuru wa Bunge, Mahakama na Tume ya Uchaguzi”.
Maoni haya siyo mageni na yamesambaa mtaani na hasa miongoni mwa viongozi wa vyama vya siasa vya upinzani. Hata hivyo, maoni kama haya yanapotolewa na ninyi viongozi wetu wakuu wa kiroho yanakuwa na mwangwi tofauti katika jamii.
Suala hili la uhuru wa Bunge na Mahakama ni mjadala wa kudumu katika siasa duniani kote. Hii inatokana na ukweli kwamba hakuna kigezo kimoja kilichokubalika duniani kote cha kupima uhuru wa Bunge na Mahakama. Kila jamii au upande una tafsiri yake kutokana na muktadha wa nchi husika.
Mheshimiwa Baba Askofu, labda nifafanue hoja yangu kwa kutumia mfano wa Bunge. Katiba yetu ipo wazi kwamba Bunge ndicho chombo cha mamlaka ya juu (supreme) katika mihimili mitatu ya dola nchini mwetu.
Aidha, katika mfumo wa vyama vingi, Bunge huongozwa kwa msingi wa demokrasia ya wachache wasikilizwe lakini wengi waamue. Katika Bunge letu la sasa, idadi ya wabunge wa chama kinachounda Serikali yaani CCM, ni zaidi ya theluthi mbili ya idadi ya wabunge wote.
Hii inamaanisha kuwa, kwa mujibu wa Katiba yetu na sheria zake, kwa Bunge hili wabunge wa CCM ndiyo wenye haki ya maamuzi kutokana na idadi yao. Kwa sababu hii, kama kuna tatizo katika mfumo wa maamuzi wa Bunge letu, tatizo la msingi haliwezi kuwa kukosekana kwa uhuru wa Bunge kwa kuwa Katiba yetu imetoa uhuru wa kutosha kabisa kwa chombo hiki. Ingekuwa ni tatizo kama kuna siku Bunge lingekuwa limeamua kinyume cha matakwa na maamuzi ya walio wengi ndani ya Bunge.
2.Kuhusu wanasiasa kuhama vyama
Mheshimiwa Baba Askofu, eneo la pili ambalo nina maoni tofauti ni katika hoja yenu ya saba linalohusu maisha ya siasa. Katika eneo hili hoja yenu ya msingi ni kwamba kuna udhalilishaji wa kauli njema isemayo “maendeleo hayana chama”. Waheshimiwa Maaskofu mnadai kuwa “udhalilishaji huu unafanyika kwa njia ya kutumia fedha nyingi katika chaguzi ndogo zinazotokana na watu wanaobadili vyama ili kuleta maendeleo”. Mmeendelea kujenga hoja kwa kujiuliza, “kama maendeleo hayana chama, kwa nini mtu anajiuzulu chama fulani eti kwenda kingine?”
Mheshimiwa Baba Askofu, katika utangulizi wa waraka wenu, mmeeleza vizuri sana kuhusu umuhimu wa kudumisha mfumo wa vyama vingi. Hata hivyo, kwa maoni yangu, kauli yenu niliyoinukuu hapo juu haikuzingatia ipasavyo utamaduni unaoambatana na mfumo wa vyama vingi.
Duniani kote, pamoja na mambo mengine, utamaduni wa mfumo wa vyama vingi huambatana na watu kuhama vyama kila wanapojisikia kufanya hivyo. Vyama vya siasa ni taasisi ambazo wanachama wake wapo huru kuingia na kutoka bila kutakiwa kujieleza kwa mtu yeyote yule ilimradi katika kufanya hivyo hawavunji sheria za nchi.
Labda nikupeni mifano michache katika kupanua uelewa wa jambo hili. Katika nchi ya jirani Kenya viongozi wote wakuu katika siasa za Kenya wamewahi kuhama vyama mara nyingi. Rais wa sasa wa Kenya ameshahama na kubadili vyama mara nne. Kiongozi nguli wa upinzani Raila Odinga ameshahama na kubadilisha vyama mara sita. Huko nchini Uganda kiongozi maarufu wa upinzani nchini humo Kiiza Besigye alikuwa katika chama kimoja na Rais Museveni, lakini alihama na kuanzisha chama chake.
Pengine unaweza ukasema tabia za kuhama vyama zipo Afrika tu. Hapana. Muasisi wa kuhama vyama duniani ni Winston Churchil, ambaye ndiye anayeshikilia rekodi ya kuwa waziri mkuu bora nchini Uingereza. Huyu alihama kutoka chama cha Conservative na kujiunga na chama cha Liberal. Baadaye tena alirudi katika chama cha Conservative na hatimaye kuchaguliwa kuwa waziri mkuu.
Ukienda nchini Marekani wapo wanasiasa maarufu 21 waliowahi kuhama vyama vyao. Kwa mfano, rais wa zamani wa Marekani Ronald Reagan alikuwa mwanachama wa chama cha Democrat, lakini alihamia chama cha Republican na baadaye akaja kuwa rais wa nchi hiyo.
Alipoulizwa kwa nini alihama alijibu kuwa “I didnt leave the Democratic Party. The party left me” (Sikukiacha Chama cha Democrat. Chama ndicho kilichoniacha). Wanasiasa wengine maarufu waliowahi kuhama vyama vyao nchini Marekani ni pamoja na Condoleeza Rice, Elizabeth Warren, Hillary Clinton na Theodore Roosevelt. Rais wa sasa wa Marekani, Donald Trump alishahama vyama mara tatu na hadi mwaka 2001 alikuwa mwanachama wa chama cha Democrat.
Mheshimiwa Baba Askofu, nimetoa mifano yote hii katika kujaribu kupanua uelewa wenu kuhusu tabia za wanasiasa katika mfumo wa vyama vingi duniani kote. Hata hivyo, jambo hili halipo katika siasa tu. Wewe unafahamu vizuri kuwa hata katika dini watu hubadili dini na madhehebu yao. Sembuse vyama vya siasa?
Aidha, katika nchi yetu tumeshakuwa na chaguzi ndogo nyingi zinazotokana na wabunge na madiwani ama kuhama vyama vyao au kufukuzwa katika vyama vyao tangu mfumo wa vyama ulipoanza, na chaguzi zote hizo husababisha gharama kubwa. Sasa ninajiuliza kwa nini Kanisa limeumia sana na chaguzi za kipindi hiki? Kuna nini?
3.Kuhusu mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu
Mheshimiwa Baba Askofu, hoja ya tatu ambayo nayo pia ningependa kuitolea maoni ipo katika eneo la tatu la waraka wenu, ambayo ni kuhusu upatikanaji wa mikopo ya elimu ya juu. Katika hoja hiyo mmeeleza kwamba, “uwezeshwaji wa vijana kupata mikopo ya elimu ya juu uwe shirikishi na usiokuwa na ubaguzi kati ya wanafunzi wa vyuo binafsi na wale wa serikali; sayansi na sanaa; wazazi maskini na wenye nafasi; waliosoma shule binafsi na wale wa shule za Serikali”.
Kwa ufahamu wangu ni kwamba kimsingi kila mkopo lazima uwe na vigezo. Msingi mkubwa wa mikopo inayotolewa kwa wanafunzi wa elimu ya juu hapa nchini ni kile kinachofahamika kama means testing, ambapo Bodi ya Mikopo huchambua maombi ya mikopo kwa kuzingatia, pamoja na mambo mengine, uwezo wa wazazi wa wanafunzi. Hivyo, mnaposema pasiwe na tofauti katika utoaji wa mikopo, mlitaka kumaanisha nini hasa?
Ni vizuri kukumbushana kuwa kuanzishwa kwa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu kulitokana na Serikali kushindwa kugharamia wanafunzi wote wanaodahiliwa katika elimu ya juu. Kwa sababu hii, njia pekee ilikuwa ni kuja na vigezo ambavyo vingewaondoa wale ambao wana uwezo wa kujilipia.
Katika mazingira haya, sio sahihi, kwa mfano, kusema kuwa hata mtoto wa mzazi mwenye wadhifa kama wangu naye apate mkopo. Aidha, kanisa haliwezi kueleweka linapotaka mtoto aliyesomeshwa na mzazi wake katika Shule ya Sekondari Feza au International School of Tanganyika naye apate mkopo wa serikali.
Aidha, kila nchi duniani ina vipaumbele vyake vya mahitaji kutokana na wakati na mazingira. Kwa wakati na mazingira ya nchi yetu kwa sasa tunahitaji zaidi wataalamu katika fani za sayansi kuliko sanaa.
Ni kwa sababu hii Serikali inawekeza zaidi katika kusomesha wanafunzi katika fani za sayansi kuliko sanaa. Huu ndiyo msingi wa Serikali kuwapa kipaumbele wanafunzi wanaosoma masomo ya sayansi kuliko wale wanaosoma masomo ya sanaa.
Kwa maoni yangu, jukumu la kanisa katika suala hili lingekuwa ni kuiasa serikali kuepuka ubaguzi katika mikopo kwa misingi ya dini, itikadi za siasa na ukabila ambapo bahati nzuri ubaguzi huo haupo.
Ubaguzi katika mikopo ya elimu ya juu kwa misingi ya uwezo wa wazazi na aina ya shule ambayo mtoto alisoma (binafsi au umma) hauepukiki. Kwa maoni yangu, kuna haja pia kuangalia kama bado ni muhimu kutoa kipaumbele kilicho sawa kati ya wanafunzi wanaodahiliwa katika vyuo vikuu vya umma na wale wanaodahiliwa katika vyuo vikuu vya binafsi.
Huo pia unaweza ukawa aina nyingine ya ubaguzi unaokubalika katika utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu, hasa katika mazingira ambayo vyuo vya umma vina nafasi ya kutosha ya kudahili wanafunzi wote wenye sifa za kujiunga na elimu ya juu.
4.Katiba Mpya
Mheshimiwa Baba Askofu, katika waraka wenu mmetoa pia maoni kuhusu umuhimu na uharaka wa kupatikana kwa Katiba mpya. Hii ni hoja kubwa inayogusa Taifa letu kwa muda mrefu. Sote tunatambua utashi na ujasiri aliouonyesha Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne wa kuruhusu mchakato huu uanze, pamoja na kwamba haikuwa ajenda ya msingi na kipaumbele katika chama chake. Kwa hiyo, ninaunga mkono kanisa kulitolea kauli jambo hili kubwa na muhimu kwa Taifa letu.
Hata hivyo, baadhi ya hoja zenu na lugha iliyotumika katika kuwakilisha hoja hiyo haiponyi bali inaligawa kanisa na nchi kwa ujumla. Kwa mfano, mnaposema kuwa “tunaisihi Serikali ya Awamu ya Tano kurejea mchakato wa upatikanaji wa KATIBA MPYA ya wananchi iliyopendekezwa na wananchi kupitia Tume ya Warioba”, mlitaka kumaanisha nini hasa?
Ninauliza hivi kwa sababu ninafahamu kuwa mchakato wa kuunda Katiba mpya ulikuwa umevuka ngazi ya Tume ya Warioba na kufikia ngazi ya Bunge la Katiba, ambapo Bunge lilipitisha kwa kura ya wengi.
Kilichokwama katika mchakato huo ni kura ya maoni ya wananchi kutokana na kukosekana kwa maridhiano mapana ya kijamii baada ya baadhi ya wawakilishi katika Bunge la Katiba kususa kuhudhuria vikao vya Bunge hilo.
Ninafahamu pia kuwa kanisa na dini zingine ziliwakilishwa kikamilifu katika Bunge hilo. Wawakilishi wa kanisa sio miongoni mwa wabunge waliosusia Bunge la Katiba, ikimaanisha kuwa kanisa liliridhia mchakato hadi mwisho na ni sehemu ya jamii waliokubaliana na rasimu iliyopitishwa na Bunge hilo.
Sababu za msingi za mchakato wa Katiba kukwama ni kutokana na kukosekana kwa mwafaka na maridhiano ya kitaifa. Kwa sababu hii mchakato wa Katiba mpya umebaki ukielea. Sasa katika mazingira haya ni hatari sana kwa ninyi viongozi wetu wakuu wa kiroho kuchukua upande mmojawapo katika mgawanyiko huo uliotokea.
Kwa maoni yangu, kwa upande wenu kama kanisa ingetosha kutoa wito wa kurejewa kwa mchakato wa Katiba mpya na kutoa wito wa mchakato huo kuzingatia maridhiano ya kitaifa.
Kwa mujibu wa matokeo ya utafiti wa Sauti za Wananchi yaliyotolewa mwezi Oktoba 2017, maoni ya wananchi yamegawanyika katika makundi manne kuhusu upatikanaji wa Katiba mpya. Kuna kundi la Watanzania linalotaka mchakato uanze upya. Kuna kundi jingine linalotaka turejee kwa Tume ya Warioba.
Lipo kundi linalotaka tumalizie mchakato kwa kwenda katika kura ya maoni. Lakini pia wapo Watanzania wanaosema hakuna haja tena ya Katiba mpya. Makundi yote haya ni ya Watanzania na bila shaka miongoni mwao ni waumini wa KKKT. Hivyo, ninyi viongozi wetu mnapoongelea suala hili kwa namna ya kuhimitisha (conclusive) mnajiweka katika mazingira ya kuchochea mgawanyiko badala ya kuleta umoja na uponyaji.
5.Kuhusu Serikali kutoendeshwa kwa ilani ya vyama
Hoja yenu nyingine katika eneo la maisha ya siasa ni kuhusu nafasi ya ilani ya vyama katika kuendesha nchi na Serikali. Katika hoja yenu hii mmenena ya kuwa, “Taifa haliongozwi na ilani za vyama. Serikali haiongozwi na ilani za vyama. Serikali huongozwa na Katiba, sheria, kanuni na mapokeo mema (misingi na tunu za Taifa)”.
Baba Askofu, niruhusu nikupeni elimu ya siasa kidogo kuhusu jambo hili. Duniani kote inajulikana kuwa chama kinachopata ridhaa ya kuunda serikali hupewa dhamana ya kutekeleza ahadi ambazo chama hicho kilizitoa katika uchaguzi.
Ndiyo kusema, vyama vinapoingia kushindana katika uchaguzi hushindania fursa ya kuunda serikali ili vitekeleze yale ambayo vinaamini ni muhimu kwa maendeleo ya Taifa husika. Kwa hivyo, msingi wa sera za serikali iliyopo madarakani ni ilani ya chama tawala iliyosheheni ahadi za chama hicho wakati wa uchaguzi.
Ndiyo kusema mara chama kinaposhinda uchaguzi na kuunda serikali ahadi zake zilizopo ndani ya ilani hugeuka kuwa ajenda za maendeleo za Taifa hilo. Ndiyo maana ahadi za CCM za uchaguzi wa mwaka 2015 ni sehemu muhimu ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano.
Kwa hiyo serikali huongozwa na vyombo vikubwa viwili katika kuendesha nchi. Chombo cha kwanza ni ilani ya chama tawala ambayo hutekelezwa kama sehemu ya ajenda za maendeleo ya Taifa husika.
Chombo cha pili ni Katiba, sheria, kanuni na miongozo mbalimbali ambayo hutolewa na vyombo mbalimbali vya dola. Katiba, sheria na kanuni ni nyenzo za utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya Taifa, ikiwemo ilani ya chama tawala.
Hadi hapo utaona kuwa hamkuwa sahihi hata kidogo kuwahubiria waumini wa KKKT na Watanzania kwa ujumla kuwa Serikali haiendeshwi kwa ilani za vyama. Ukweli ni kuwa ilani ya chama tawala ni nyenzo na ajenda muhimu ya kuendesha serikali katika nchi zote zinaendeshwa kidemokrasia na kwa kufuata utawala wa sheria.
Marekani, kwa mfano, leo wanajenga ukuta wa kuitenga Marekani na Mexico ili kudhibiti wahamiaji kutoka Mexico. Hii ilikuwa ni moja ya ahadi kubwa za Rais Donald Trump na chama chake cha Republican wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2016. Baada ya Donald Trump kushinda uchaguzi na kuunda serikali ahadi hii sasa ni ajenda ya Taifa la Marekani.
Mheshimiwa Baba Askofu, nihitimishe barua yangu kwa kurudia tena pongezi za dhati kwa kuandaa Waraka ambao umegusa masuala nyeti yanayohusu nchi yetu. Hata hivyo, upo umuhimu kwa kanisa kujiepusha kadri inavyowezekana kuonekana lipo upande fulani kwenye mijadala ya kitaifa inayogusa jamii pana yenye mitazamo kinzani.
Kwa kufanya hivyo, mtaepusha migawanyiko isiyo ya lazima kwa waumini ndani ya kanisa na wananchi kwa ujumla. Ushauri wangu ni kwamba ili kanisa lionekane linaendeleza kazi za msingi zilizoanzishwa na Bwana wetu Yesu Kristo, ni muhimu sana kufanya utafiti na uchambuzi wa kina wa jambo lolote kabla ya kulitolea kauli hadharani.
Aidha, ni muhimu kwa kanisa kupima kwa umakini mkubwa uzito wa kila neno kabla ya kutoa kauli katika umma. Ni hatari kwa kanisa kutoa kauli inayosababisha maumivu na mifarakano badala ya kuponya. Ili kuepuka kauli za namna hii, ni vizuri kila mara kanisa na viongozi wetu mkajenga hoja zenu kwa kuzingatia mantiki na ushahidi wa kiinjili unaopatikana ndani ya Biblia Takatifu, na/au mantiki na ushahidi wa kisayansi unaopatikana kupitia tafiti na tafakuri pana na shirikishi.
Mheshimiwa Baba Askofu, Bwana Yesu Asifiwe.
Kwa heshima na taadhima ninaomba kuwasilisha.
Dodoma
Alhamisi 29 Machi 2018.
Maoni
Chapisha Maoni