Uhakika media 5 · 4 hours ago
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimefunguka na kudai hakijawahi kushindwa uchaguzi wowote ule ambao umefanyika katika ardhi ya Tanzania bali kinachowapata ni kupokwa matokeo yao na kurundikwa katika chama kingine cha siasa.
Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Baraza la Vijana CHADEMA (BAVICHA), Patrick Ole Sosopi wakati alipokuwa anazungumza kwenye media tour yake leo Juni 08, 2018 Jijini Dar es Salaam na kusema ushahidi wa jambo hilo ni mmoja wapo ni uchaguzi wa mdogo wa marudio katika Jimbo la Kinondoni ambapo sanduku la kuwekea kura liliibwa mbele ya askari polisi na likarudishwa huku kukiwa hakuna mtu yoyote aliyekamatwa.
"Nataka kuwahakikishia watanzania kwamba CHADEMA iko imara kuliko jana, kuzuiwa kwa mikutano ya kisiasa ndio inaathari kwa sababu kazi yetu ni siasa,upande wa pili anatuimarisha zaidi sababu nyuma ya pazia kila mtanzania anajua ukweli", amesema Sosopi.
Pamoja na hayo, Sosopi ameendelea kwa kusema "kuzuiliwa kwa mikutano ya Vyama vya Siasa ni kuua vipaji na vijana kushiriki kwenye shughuli za siasa, kwa sababu vijana wametiwa hofu, vijana wametumia mitandao ya kijamii huko wamekutana na sheria za mitandao Cybercrime),Rais anazuia watu kufanya siasa wakati yeye ni Mwenyekiti wa CCM anafanya siasa, anakataza siasa vyuoni wakati wao wanaratibu na wana vitengo maalum vya kufanya siasa vyuoni".
Kwa upande mwingine, Sosopi amesema wao kama CHADEMA hawatopambana tena na Chama cha Mapinduzi (CCM) na badala yake watapambana na dola.
Maoni
Chapisha Maoni