Uhakika media 5 · 1 hour ago
INSPEKTA Jenerali wa Polisi, Simon Sirro, jana alisema askari wake katika mikoa yote nchini wamepangwa kikamilifu kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama kuhakikisha kuwa sikukuu ya Pasaka inasherehekewa kwa amani na utulivu.
IGP Sirro alisema polisi watahakikisha hakuna vitendo vyovyote vya uhalifu vitakavyofanyika na pale vitakapojitokeza vitadhibitiwa kwa haraka.
Katika mkakati huo, IGP Sirro alisema, ulinzi utaimarishwa kwenye maeneo yote yakiwemo maeneo ya kuabudia, fukwe, sehemu za starehe na maeneo mengine ambayo yatakuwa na mikusanyiko mikubwa ya watu ili kuhakikisha wananchi wote wanasherehekea sikukuu hiyo katika hali ya utulivu.
Aidha, IGP Sirro alitahadharisha wale wote ambao watakuwa wakitumia barabara kuwa makini na kuzingatia sheria za Usalama Barabarani.
Alitaka madereva wa magari na pikipiki kuepuka kujaza watu kupita kiasi, kubeba mishikaki, kwenda mwendo kasi, kutumia vilevi pamoja na kupiga honi ovyo.
Katika salamu zake hizo kwa ajili ya siku kuu hiyo ya Jumapili ikianza na maombolezo ya Ijumaa Kuu kesho, IGP Sirro aliwashukuru wananchi kwa ushirikiano wanaoendelea kuutoa kwa Jeshi la Polisi.
Alisema ushirikiano huo umesaidia kupunguza uhalifu kwa kiasi kikubwa hapa nchini, "Kiujumla hali ya usalama hapa nchini ni shwari na matukio makubwa ya uhalifu wa kutumia silaha (bunduki) yamepungua kwa kiasi kikubwa," alisema IGP katika salamu hizo kwa njia ya waraka na kueleza zaidi:
"Jitihada za kukabiliana na makosa ya usalama barabarani zinaendelea ili kupunguza ajali zinazosababisha vifo na majeruhi kwa raia.
"Wazazi wanatakiwa kuwaangalia watoto wao na kutowaacha kutembea peke yao bila ya kuwa na uangalizi wa karibu.
"Pia wamiliki wa kumbi za starehe wanatakiwa kufuata sheria, kanuni na taratibu za uendeshaji wa kumbi hizo, ikiwemo kutoruhusu disko toto na kujaza watu kupita kiasi.
"Nawatakia Pasaka njema."
Maoni
Chapisha Maoni