DC aitaka halmashauri kufadhili mkaa endelevu
Uhakika media / 4 hours ago
Mkuu wa wilaya ya Kilosa, Adam Mgoi (wa pili kulia), akizunguza katika moja ya mikutano ndani ya wilaya yake.
Suleiman Kasei, Kilosa
MKUU wa wilaya (DC)ya Kilosa, Adam Mgoi amelitaka Baraza la Madiwani la halmashauri hiyo kuteua kijiji cha mfano ili iweze kuanzisha na kufadhili mradi unaohamasisha wananchi kulinda misitu yao unaojulikana zaidi kama mkaa endelevu.
Akizungumza baada ya kutembelea mradi wa aina hiyo katika kijiji cha Kitunduweta, Tarafa ya Uyala, Kilosa, unaofadhiliwa na mashirika yasiyo ya kiserikali juzi, Mgoyi, amesema mradi huo utafanyika katika mwaka wa fedha 2018/19 baada ya baraza kupitisha.
Mkuu wa wilaya amesema halmashauri hiyo itajielekeza katika maeneo ambayo ni hatari katika kuharibu misitu hususan maeneo ya Kaskazini mwa wilaya ya Kilosa, kuanzia eneo la Mbaku, Kwambe na vijiji vingine ambavyo vitaonekana kuharibika.
“Ili kuunga mkono jitihada za Mradi wa Kuleta Mageuzi katika Sekta ya Mkaa (TTCS), mwaka ujao, halmashauri itakuwa na kijiji ambacho na wao watakifanya kuwa cha mfano kwa sababu tuna walimu wa kutosha kutoka vijiji 20 vilivyopo kwenye mradi,” amesema.
Mgoi amesema pamoja uanzishaji wa kijiji cha mfano amevitaka vijiji vinavyotekeleza mradi kuendelea kubuni mbinu mbalimbali za kuongeza mapato ili kusaidia Serikali kuleta maendeleo.
Amesema ofisi yake itatoa ushirikiano kwa kijiji chochote ambacho kitatumia fedha za mradi katika miradi ambayo inahitajika kwa jamii kama ujenzi wa zahanati, shule na mingine.
Mgoi amesema mradi wa mkaa endelevu una manufaa makubwa kwani unaipunguzia pia halmashari mzigo na hivyo akaahidi kuona mradi huo unasambaa.
Ofisa Mtendaji wa kijiji hicho, Margaret Magele, amesema mradi huo umechangia katika kukiwezesha kijiji kujenga ofisi ya kisasa, kukarabati madarasa mawili na ujenzi wa nyumba ya mwalimu ambayo imefikia hatua za mwisho kukamilika.
“Mradi wa TTCS umekuwa msaada mkubwa sana kwani kati ya sh. milioni 16.5, milioni 9.2 zimetumika katika miradi ya maendeleo na tunatarajia katika mwaka wa fedha 2018/19 tutatupanga bajeti mpya kwa miradi mingine,” amesema.
Magele ameongeza pia kijiji kupitia mradi kimefanikiwa kufungua kikundi hisa chenye wanachama 87 na mtaji wa sh. milioni 31, kilimo hifadhi wanakijiji 37 na wachomaji mkaa endelevu 60.
Meneja mradi huo wa TTCS, Charles Leonard, amesema mradi wa kuzalisha mkaa endelevu unaendeshwa na Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania (TFCG) kwa kushirikiana na Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania (MJUMITA) pamoja na Shirika la Kuendeleza Nishati Asilia (TaTEDO) chini ya ufadhili wa Shirika la Maendeleo na Ushirikiano la Uswisi (SDC).
Amefafanua kuwa mradi huo unaotekelezwa na vijiji 30 katika wilaya za Morogoro, Kilosa na Mvomero umeweka mpango mzuri wa matumizi ya misitu na pia kuzalisha mkaa bila kuathiri misitu huku wananchi, kijiji na serikali vikinufaika na uvunaji huo wa raslimali za misitu.
Maoni
Chapisha Maoni