Uhakika media5 · 1 hour ago
Nahodha wa Taifa Stars ambaye anayekipiga kwenye klabu ya KRC Genk ya Ubelgiji, Mbwana Samatta amesema ipo haja ya kuwepo mechi za kirafiki nchini kwa madai kitendo hicho kitapelekea kuwajenga vizuri wachezaji wa ndani pamoja na kuwapa uzoefu mkubwa.
Samatta ametoa kauli hiyo muda mchache ilipomalizika mechi yao dhidi ya DR Congo (The Leopards) kwenye mchezo wa kirafiki wa kalenda ya FIFA kwa mwezi Machi uliomalizika ikiwa Stars wamepata ushindi wa mabao 2-0 mtanange uliyochezwa kwenye uwanja wa taifa Jijini Dar es Salaam.
"Mechi hizi za kirafiki nafikiri Tanzania wanazihitaji kwa sana japokuwa ni 'game' ngumu lakini mwisho wa siku unapopata matokeo mazuri yanasaidia kukusogeza kwa kiasi fulani katika viwango vya FIFA, pia hata usipopata matokeo mazuri yanaweza kukusaidia kukujenga katika kujiamini na uzoefu zaidi", amesema Samatta.
Pamoja na hayo, Mbwana Samatta ameendelea kwa kusema "ni michezo ambayo tunaihitaji katika kuwajenga wachezaji wetu wa tanzania hata ikitokea tukakutana nao katika mashindano inatusaidia kupata matokeo mazuri kutokana na uzoefu".
Kwa upande mwingine, Samatta amesema anatamani kuwaona wachezaji wengi kujitokeza katika kuijenge timu ya Taifa ili izidi kuwa bora zaidi.
Maoni
Chapisha Maoni