Tundu Lissu awakumbusha viongozi wa dini kuzungumzia ukandamizaji haki
Uhakika media / 1 day ago
Tundu Lissu
Suleiman Kasei
MBUNGE wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), amewataka maaskofu, mashekhe, wachungaji, mapadri, wainjilisti, maimamu na wananchi kwa ujumla waamke kulaani vikali vitendo anavyodai vya ukandamizaji wa haki za binadamu.
Lissu ameyasema hayo ikiwa ni siku chache baada ya Mchungaji wa Kanisa la Kiinjilisti la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kilimanjaro Kati, Fred Njama kuhojiwa na Jeshi la Polisi mkoani humo.
Pamoja na Jeshi la Polisi kutosema sababu za kumkamata Mchungaji Njama, tukio la kukamatwa na kuhojiwa kiongozi huyo linakuja ikiwa ni siku chache baada ya kutoa taarifa ya kanisa lake kwa waamini ambapo aliaonisha changamoto mbalimbali zilizopo nchini kwa sasa.
Kwa mujibu wa video ambayo imesambaa mitandaoni ikimuonesha Mchungaji Njama anasema uchumi haujaimarika na umaskini unaendelea kuongezeka kwa nguvu.
“Umaskini umendelea kuongezeka kwa nguvu, tumeshuhudia biashara nyingi zikifungwa, wakulima wamekata tamaa na gharama za uzalishaji zimekuwa kubwa sana,” amesema.
Pia mchungaji huyo ameongeza kuwa serikali haitoi ruzuku ila wakati wa kuuza mazao wakulima hawana uhuru wauze wapi kwa bei gani, wafugaji pia wanazalisha kwa gharama kubwa.
Akizungumzia hali hiyo Lissu amesema kwa matukio ambayo yametokea takribani miaka miwili sasa ni wazi kuwa kila mwanajamii anapaswa kunyanyuka na kuachana na dhana ya kundi fulani kwani yote yameguswa.
“Maaskofu, wachungaji, mapadri, wainjilisti, mashehe, maimamu na kila aina ya kiongozi wetu wa kidini, waamke na kulaani vikali vitendo hivi vya ukandamizaji wa haki za binadamu za viongozi wa kiroho kutoa maoni yao hadharani na kukemea maovu ya utawala huu,” amesema.
Amefafanua kuwa ni wakati sasa wa waumini wao kuunga mkono na kushikamana nao na vyama vyetu vya siasa, taasisi za kiraia na kitaaluma na vyombo vya habari, navyo vipige kelele.
“Kelele ya umma dhidi ya ukandamizaji ni kelele ya Mungu. Kimya mbele ya ukandamizaji ni kuunga mkono ukandamizaji,” amesema.
Amefafanua kuwa pamoja na ukweli kwamba aliyekamatwa ni kiongozi wa kidini, lakini sio viongozi wa kiroho peke yao wanaotakiwa kulaani ukandamizaji wa aina hii wa haki za binadamu na kuwa ni jambo la kila mmoja wetu.
Mbunge huyo amesema haki za binadamu ni za watu wote pamoja na viongozi wa kidini na ukandamizaji wa haki hizo kwa mtu mmoja ni ukandamizaji wa haki hizo kwa watu wote.
Lissu ambaye yupo nchini Ubelgiji kwa matibabu baada ya kushambuliwa kwa risasi 32 akiwa nyumbani kwake mjini Dodoma na watu wasiojulikana amesema ni miaka miwili iliyopita alisema hali hii inapaswa kupingwa na kila mwenye akili timamu lakini inawezekana hakueleweka.
“Tangu niyaseme maneno haya mahakamani Kisutu Juni 29 mwaka 2016, ni watu wangapi wameuawa, kupotezwa, kuumizwa, kukamatwa na kufunguliwa mashtaka ya 'uchochezi' au mengineyo ya ajabu ajabu,” amehoji.
Amesema ni watu wangapi wamepoteza ajira zao, makazi yao, mali zao nyingine kutokana na matumizi ya ovyo ya madaraka ya utawala ulioko madarakani.
Kwa upande wake Msemaji wa Jumuiya na Taasisi za Kiislam Tanzania, Sheikh Rajab Katimba amesema kuna mahali taifa limekengeuka hali ambayo inatoa picha mbaya kwa jamii.
Katimba amesema viongozi wa Serikali wanapaswa kukaa na viongozi wale wa dini kuhakikisha jitihada za kusukuma gurudumu la maendeleo zinafanyika kwani kuwepo kwa mazingira ambayo yanaonekana kwa sasa sio afya nzuri kwa nchi.
“Tunatakiwa kukaa na kutafakari kinachoendelea nchini kwa sasa haya ambayo yanatokea sasa sio tamaduni zetu naamini tunapaswa kubadilika kwa maslahi ya Tanzania na Watanzania,” amesema.
Ameongeza kuwa viongozi wa dini na Serikali wanapaswa kufanya kazi pamoja kinyume cha hapo Taifa litaenda kusikohitajika kwani heshima ya viongozi wa dini inatakiwa kubakia pale pale.
Mwenyekiti wa jumiya hiyo Sheikh Mussa Kundecha, amewataka viongozi kutambua kuwa hakuna mtu mkamilifu hivyo wawe tayari kukosolewa pale inapobidi.
Kundecha amesema iwapo kila kiongozi ataishi katika misingi hiyo hakuna ambaye ataona kuwa ananyimwa raha na upande wowote huku akivitaka vyombo vya habari kutenda haki katika kuelimisha jamii.
Mtume Onesmo Ndegi, wa Kanisa la Living Waters Centre jijini Dar es Salaam, amesema taarifa hizo amezisikia ila hajapata undani wake na kwamba anataka kuzifanyia kazi ili aweze kuzungumza katika haki bila kumtuhumu mtu au taasisi.
Maoni
Chapisha Maoni