VIONGOZI sita wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wakiongozwa na Mwenyekiti wao, Freeman Mbowe, wamewataka Watanzania na wanachama wao wasiogope kwa sababu katika kupigania haki, demokrasia, amani na ustawi wa nchi lazima wapatikane watakaoumia kwa ajili ya wengine.
Ujumbe huo wameutoa wakiwa ndani ya Gereza la Segerea, Dar es Salaam jana ikiwa ni siku moja imepita baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuamuru viongozi hao wafikishwe mahakamani Aprili 3, mwaka huu ili kutimiza masharti ya dhamana zao baada ya juzi kudaiwa kushindwa kufikishwa kutokana na gari kuwa bovu.
Ujumbe huo wa Mbowe na viongozi wenzake ulitolewa jana na Mbunge wa Rombo (Chadema), Joseph Selasini na kada wa chama hicho, Dk. Makongoro Mahanga, waliopata muda wa nusu saa kuzungumza mambo mbalimbali na viongozi hao.
Selasini na Mahanga waliweka ujumbe huo katika akaunti zao za mtandao wa Facebook, pamoja na mambo mengine walisema wamewaona viongozi na haya ndiyo maneno yao: ‘Tuko imara, tuko vizuri. Wapelekeeni wenzetu ujumbe huu. Msiogope. Taifa linatutegemea. Chadema ndiyo pekee itakayobadilisha uonevu unaofanywa na watawala kwa Watanzania na kuwahakikishia demokrasia, amani ya kweli, haki na maendeleo. Tukiwa waoga tutakuwa wasaliti wa matamanio hayo ya Watanzania.’
“Wamesema pia wamepata muda mzuri wa kupumzika na kufanya retreat (tafakari ya kina. Tumemkuta Mbowe akiwa na Biblia mkononi. Amesema amesoma na karibu anamaliza Injili zote. Pia yeye pamoja na Mchungaji Peter Msigwa, Mbunge wa Iringa Mjini leo (jana) wataadhimisha ibada ya Ijumaa Kuu kwa kuwashirikisha mahabusu na wafungwa wote wao kama watumishi wa neno la Mungu.”
MTANZANIA Jumamosi lilizungumza na Selasini kwa njia ya simu na alithibitisha kuwa ujumbe huo ni wake na kusisitiza kuwa walisema Watanzania wasiogope.
EU KUZUNGUMZA NA SERIKALI
Katika hatua nyingine, Selasini aliliambia MTANZANIA Jumamosi kuwa Mabalozi wa Umoja wa Ulaya (EU), wamewaahidi kukutana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi Dk. Augustine Mahiga, ili kuzungumza naye kuhusu mwafaka wa hali ya kisiasa nchini.
Alisema wabunge 40 Chadema walikutana na mabalozi wa EU na kuzungumza nao kwa saa nne ili kuwafahamisha namna mihimili ya dola inavyopambana na upinzani.
“Ni kama mhimili mmoja unapambana na mhimili mwingine, hivyo ni lazima tutafute namna ambayo watu wanaweza kushauri au kuingilia kati, kwa sababu sasa hivi vyombo vya habari vimebanwa, watu wanatekwa na wengine kuuawa, hofu imetanda katika jamii huku dunia ikiwa haijui.
“Hivyo tulichofanya ni kutaka wajue ili waweze kushauri au kufikisha ujumbe kwa dunia, sisi tulipeleka ujumbe kutokana na matukio yanayotokea ambayo hayafanyiwi uchunguzi na kuvuruga amani ambayo tumedumu nayo kwa muda mwingi. Na sasa Serikali iliyopo haisikilizi wala kushaurika,” alisema.
Dhamana ya Mbowe na wenzake
Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Wilbard Mashauri, alitoa uamuzi wa kuwapa dhamana washtakiwa bila wenyewe kuwapo kwa masharti kwamba wawe na wadhamini wawili kila mmoja wenye barua na vitambulisho, wasaini dhamana ya maandishi ya Sh milioni 20 na washtakiwa wanatakiwa kuripoti polisi kila Alhamisi.
MASHTAKA
Washtakiwa wote wanadaiwa kufanya mkusanyiko au maandamano yasiyo halali, kuendelea na mkusanyiko usio halali wenye vurugu baada ya kutolewa tamko la wao kutawanyika.
Mbowe peke yake alisomewa mashtaka ya kuhamasisha chuki miongoni mwa wanajamii isivyo halali, uchochezi na kusababisha chuki miongoni mwa wanajamii, uchochezi wa uasi, ushawishi utendekaji wa kosa huku Msigwa akisomewa shtaka la kushawishi raia kutenda kosa.
Washtakiwa wote Februari 16, mwaka huu, wakiwa katika Barabara ya Kawawa, Kinondoni Mkwajuni, Dar es Salaam kwa pamoja wakiwa wamekusanyika kutekeleza lengo la pamoja kinyume cha sheria, waliendelea na mkusanyiko katika namna iliyowafanya watu waliokuwa katika eneo hilo waogope watakwenda kwenye uvunjifu wa amani.
Inadaiwa washtakiwa wote katika tarehe hiyo wakiwa kwenye barabara hiyo kwa pamoja katika ujumla wao wakiwa
Maoni
Chapisha Maoni