UGONJWA WA SARATANI YA SHINGO YA KIZAZI NA NAMNA YA KUJIKINGA
March 27,02018 by uhakika media
SARATANI ya shingo ya kizazi ni aina ya saratani ambayo hushambulia sehemu ya viungo vya uzazi vya mwanamke inayounganisha kati ya uke na mfuko wa mimba (uterus). Ugonjwa huo husababishwa na virusi vya HPV(human papilloma virus).
Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya Duniani (W.H.O), saratani ya shingo ya kizazi ni saratani inayoongoza kwa kusababisha vifo vya wanawake wengi duniani. Inakadiriwa kuwa asilimia 85 ya vifo hivi hutokea katika nchi zinazoendelea.
Mwanamke anapopata maambukizi ya HPV(Human Papilloma Virus), kwa mara ya kwanza kinga yake hujaribu kupambana na virusi hawa ili wasilete madhara,virusi hawa wasipodhibitiwa mapema
huanza kushambulia seli za shingo ya kizazi na kusababisha ukuaji wa seli za saratani katika eneo hili.
VIHATARISHI VYA SARATANI YA SHINGO YA KIZAZI
Zipo sababu nyingi zinazoweza kusababisha mtu akapata ugonjwa wa saratani ya shingo ya kizazi. Baadhi ya sababu hizo ni:
– Kuanza kufanya ngono mapema katika umri mdogo: Wanawake wanaoanza kujamiana wakiwa na umri wa miaka 16 au chini ya hapo, wapo kwenye hatari ya baadaye kuja kupata saratani ya shingo ya kizazi.
– Kuwa na wapenzi wengi: Mwanamke mwenye wapenzi wengi au mwenye mwanamume mwenye wapenzi wengi yupo kwenye hatari ya kupata ugonjwa huu. Utumiaji wa kondomu hupunguza hatari ya kupata saratani hii, lakini ikumbukwe ya kwamba kondomu sio kinga ya ugonjwa huu.
– Maambukizi ya humanpapilloma virus.
– Uvutaji wa sigara: Kemikali zilizopo kwenye sigara huchanga-nyikana na seli au chembe-chembe za shingo ya kizazi hivyo kuleta mabadiliko katika shingo ya kizazi hatimaye kusababisha saratani.
– Utumiaji wa vidonge vya kupanga uzazi kwa muda mrefu hasa wale wanaotumia kwa zaidi ya miaka mitano (miaka 5).
– Kuzaa watoto wengi: Wanawake ambao wamepata watoto zaidi ya watano wako kwenye hatari kubwa sana ya kupata saratani ya shingo ya kizazi. Ndio maana mama akishafikisha watoto watano anashauriwa kufunga kizazi.
– Umri mkubwa: Baada ya kufikisha umri wa miaka 25, hatari ya kupata saratani hii huongezeka. Wanawake wenye zaidi ya miaka 45 wako kwenye hatari zaidi ya kupata saratani ya shingo ya kizazi.
– Upungufu wa kinga mwilini: Magonjwa yanayosababisha upungufu wa kinga mwilini kama Ukimwi huchangia kupata saratani ya shingo ya kizazi. Hata baadhi ya dawa pia husababisha upungufu wa kinga mwilini, mfano, dawa zinazotolewa baada ya mgonjwa kupewa kiungo cha mtu mwengine kama figo,moyo nk.
– Historia ya saratani ya shingo ya kizazi katika familia. Saratani hii pia inahusishwa na kiashiria cha aina ya HLA-B7 ambacho kinaweza kurithishwa kwenye familia ya mgonjwa wa saratani ya shingo ya kizazi.
Maoni
Chapisha Maoni