Watu 53 wafariki katika mkasa wa moto jumba la Kemerovo, Urusi
Uhakika media / 19 hours ago
WATU 53 wamethibitishwa kufariki dunia baada ya moto kuzuka katika jumba moja kubwa la kibiashara katika mji maarufu kwa uchimbaji wa mkaa wa mawe wa Kemerovo, eneo la Siberia nchini urusi.
Watu zaidi ya 64 hawajulikani walipo, wakiwemo watoto 41. Baadhi ya maeneo ya jumba hilo kubwa yanadaiwa kuwa kwenye hatari ya kuporomoka.
Moto huo ulianza katika ghorofa ya juu katika jumba Winter Cherry.Inadaiwa wengi wa waliofariki walikuwa kwenye kumbi za sinema.
Video zilizopakiwa mitandao ya kijamii zinawaonesha watu wakiruka nje kupitia madirisha kujaribu kujinusuru kutoka kwa moto huo uliozuka jana Jumapili.
Zimamoto zaidi ya 660 wametumwa kusaidia juhudi za uokoaji.Chanzo cha moto huo hakijabainika lakini maofisa wameanzisha uchunguzi. Kemerovo, ni eneo maarufu kwa uchimbaji wa mkaa wa mawe.
Ni mji unaopatikana takriban kilomita 3,600 mashariki mwa mji mkuu Moscow. Kansela wa Austria Sebastian Kurz ametuma salamu zake za rambirambi kwa jamaa na marafiki wa waathiriwa, sawa na Waziri wa mambo ya nje wa Latvia Edgars Rinkēvičs.
Moto ulianza vipi?
Kando na kumbi nyingi za sinema, jumba hilo, ambalo lilifunguliwa mwaka 2013, lina migahawa kadha, na vituo kadha vya bafu za maji ya mvuko, kito cha mchezo wa bowl na kituo cha kujumuika na wanyama.
Moto unaaminika kuanza mwendo wa saa 17:00 (10:00 GMT) kwenye sehemu ya jengo hilo ambayo ina kumbi za burudani, vyombo vya habari Urusi vinasema.
"Uchunguzi wa awali unaonesha kwamba dari liliporomoka katika kumbi mbili za sinema," Kamati ya Uchunguzi ya Urusi imesema kupitia taarifa.
Yevgeny Dedyukhin, naibu mkuu wa idara ya huduma za dharura katika eneo la Kemerov, wamesema eneo ambalo liliathiriwa na moto huo ni la ukubwa wa mita 1,500 mraba.
"Jumba hili limejengwa kwa njia ambayo inatatiza juhudi za kudhibiti moto," alisema.
"Kuna vitu vingi ambavyo vinaweza kushika moto."
Tunafahamu nini kuhusu waathiriwa?
Miili ya watu 37 ambayo ilikuwa imeungua kiasi cha kutotambulika imegunduliwa, kwa mujibu wa Dedyukhin huku tisa kati ya waliofariki ni watoto.
Andrei Mamchenkov, naibu mkuu wa Kituo cha Kudhibiti Mikasa cha Taifa hilo, amesema shughuli ya kuwatafuta watoto 41 inaendelea.
Maofisa wa kuzima moto wameshindwa kufikia moja ya kumbi za sinema zilizokuwa kwenye ghorofa ya tatu juu ya moshi na hatari ya jengo kuporomoka, ofisa mmoja ambaye hakutaka jina lake litajwe amenukuliwa na shirika la habari la Urusi la Interfax.
Mdokezi mwingine ameambia shirika hilo kwamba kwa sasa hawatarajii kupata manusura.
Maoni
Chapisha Maoni