Uhakika media 1 · 1 hour ago
Washiriki wa mafunzo kutoka Mikoa 13 Nchini wakifuatilia mada mada zilizokuwa zikitolewa na makufunzi wa mafunzo ya mfumo wa uzalishaji mbegu kupitia mradi wa “Mbegu Zetu Haki Zetu” yaliyofanyika mwishoni mwa wiki Mkoani Morogoro na kuandaliwa na Shirika la PELUM Tanzania kupitia ufadhili wa Bread for the World
Akizungumza mwishoni mwa wiki Mkoani Morogoro katika mafunzo ya mfumo wa uzalishaji mbegu kupitia mradi wa “Mbegu Zetu Haki Zetu” yaliyoandaliwa na Shirika la PELUM Tanzania kupitia ufadhili wa Bread for the World, Mratibu toka Shirika la TABIO Abdallah Mkindi alisema, uundaji wa chombo cha kisheria katika mfumo wa mbegu usio rasmi utasaidia kuleta mageuzi ya haraka katka sekta ya kilimo nchini.
“Mfumo huu wa mbegu usio rasmi unatumiwa na zaidi ya asilimia 70 ya wakulima wote nchini hivyo basi Serikali inapaswa kushirikiana na wadau mbalimbali wa kilimo kuendeleza mfumo huu kuanzia hatua ya uchaguzi wa mbegu, uhifadhi pamoja na tafiti shirikishi,” alisema Mkindi.
Mkindi alisema ili mfumo huo uweze kuleta tija iliyokusudiwa ni Serikali pia itapaswa kusimamia uanzishwaji na uimarishwaji wa benki za mbegu na hasa zile zinazopotea pamoja na kuimarisha mfumo wa usimamizi katika utafiti wa mbegu za asili zilizopo, zinazopotea na zilizopotea ili kuweza kuzirudisha.
Kwa mujibu wa Mkindi aliitaka Serikali pia kuongeza nguvu ya ushirikiano na kituo cha uhifadhi wa nasaba za mimea (NPGRC) ili kujua nasaba zilizohifadhiwa katika kituo hicho na namna zinavyoweza kuwafikia wakulima pale zinapohitajika.
Kwa upande wake Afisa kilimo, kutoka Kituo cha Kilimo LAELA la Mkoani Rukwa, Gaudens Masebe alisema mfumo usio rasmi wa mbegu unapaswa kuwa na mtaala maalum katika shule za msingi na sekondari pamoja na taasisi za elimu ya juu nchini kwa kuwa moja ya faida ya mbegu hizi ni kuwa zinakabaliana na mazingira anayotoka mkulima na ni rahisi kuhifadhi kwa njia za asili zisizo na gharama.
Naye Herman Hishamu, Meneja Miradi, kutoka Shirika la Island of Peace la Mkoani Arusha alisema mbegu toka mfumo ulio rasmi zimekuwa na changamoto nyingi kwa wakulima ikiwemo kutokuwepo na uhakika wa mbegu hizo kuota jambo ambalo kila mwaka mkulima anabadili mbegu kwenye shamba moja.
Aidha waalibainisha changamoto nyingine ambazo wakulima wanazipata wanapotumia mfumo rasmi wa mbegu ambapo pamoja na mkulima kununua mbegu bado atapaswa kununua mbolea kuweka shambani na pia kunyunyuzia madawa kwa ajili ya kuulia wadudu na kuzuia magonjwa.
Aidha Francis Mwitumba Meneja Programu kutoka Shirika la Caritas Mbeya alibainisha kuwa mfumo wa mbegu usio rasmi unamshirikisha moja kwa moja mkulima toka eneo husika kufahamu hatua zote za uzalishaji mbegu kupitia mazingira anayoishi, uchaguzi na uhifadhi wa mbegu na kupata uhakika wa kuvuna mbegu kwa wakati husika na kwa bei nafuu.
Mradi wa “Mbegu zetu Haki zetu” unaotekelezwa na Shirika la PELUM Tanzania kupitia Masharika wanachama 20 toka Mikoa 13 nchini na unatarajia kukamilika mwaka 2020. Unasisistiza juu ya mfumo usio rasmi wa mbegu ambapo kaya 400 (wakulima)toka mashirika wanachama watanufaika mojamoja na mradi huu
Maoni
Chapisha Maoni